Genesis 25

Kifo Cha Ibrahimu

1Ibrahimu alioa mke mwingine, ambaye jina lake aliitwa Ketura. 2 aHuyu alimzalia Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. 3Yokshani alikuwa baba wa Sheba na Dedani, wazao wa Dedani walikuwa Waashuri, Waletushi na Waleumi. 4 bWana wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa. Hawa wote walikuwa uzao wa Ketura.

5 cIbrahimu akamwachia Isaka kila kitu alichokuwa nacho. 6 dLakini Ibrahimu alipokuwa bado hai, akawapa watoto wa masuria wake zawadi, kisha akawaondoa waende kuishi pande za mashariki mbali na mwanawe Isaka.

7 eKwa jumla, Ibrahimu aliishi miaka 175. 8 fNdipo Ibrahimu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku, naye akakusanywa pamoja na watu wake. 9 gWatoto wake Isaka na Ishmaeli wakamzika katika pango la Makpela karibu na Mamre, katika shamba lililokuwa la Efroni mwana wa Sohari Mhiti, 10 hShamba ambalo Ibrahimu alilinunua kwa Wahiti. Hapo ndipo Ibrahimu alipozikwa pamoja na mkewe Sara. 11 iBaada ya kifo cha Ibrahimu, Mungu akambariki mwanawe Isaka, ambaye baadaye aliishi karibu na Beer-Lahai-Roi.

Wana Wa Ishmaeli

12 jHivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli mtoto wa Ibrahimu, ambaye mjakazi wake Sara, Hagari Mmisri, alimzalia Ibrahimu.

13 kHaya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, yaliyoorodheshwa kulingana na jinsi walivyozaliwa: Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli ni Nebayothi, akafuatia Kedari, Adbeeli, Mibsamu, 14 lMishma, Duma, Masa, 15 mHadadi, Tema, Yeturi, Nafishi na Kedema. 16 nHawa walikuwa wana wa Ishmaeli na haya ni majina ya viongozi wa makabila kumi na mawili kulingana na makao yao na kambi zao. 17Kwa jumla Ishmaeli aliishi miaka 137. Akapumua pumzi ya mwisho, akafa, naye akakusanywa pamoja na watu wake. 18 oWazao wa Ishmaeli waliishi kuanzia nchi ya Havila hadi Shuri, karibu na mpaka wa Misri, unapoelekea Ashuru. Hao waliishi kwa uhasama na ndugu zao wote.

Yakobo Na Esau

19Hivi ndivyo vizazi vya Isaka mwana wa Ibrahimu.

Ibrahimu akamzaa Isaka,
20 pIsaka alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu.

21 qIsaka akamwomba Bwana kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. Bwana akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba. 22 rWatoto wakashindana tumboni mwake, akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza Bwana.

23Bwana akamjibu, “Mataifa mawili yamo tumboni mwako,
na mataifa hayo mawili
kutoka ndani yako watatenganishwa.
Mmoja atakuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine,
na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”

24Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake. 25Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina lake Esau.
Esau maana yake Mwenye nywele nyingi.
26Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina lake Yakobo.
Yakobo maana yake Ashikaye kisigino, au Atwaaye mahali pa mwingine, au Mdanganyaji, au Mwenye hila, au Mlaghai, au Mjanja.
Isaka alikuwa mwenye miaka sitini Rebeka alipowazaa.

27Watoto wakakua, naye Esau akakuwa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, wakati Yakobo alikuwa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani. 28Isaka, ambaye alikuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo.

29Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu, Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali. 30Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu.)
Edomu maana yake Mwekundu.

31Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”

32Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu ya kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?”

33Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya kuzaliwa.

34Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu. Akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake.

Kwa hiyo Esau alidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Copyright information for SwhKC